Friday, 10 October 2014

TAHADHARI ! UGONJWA MPYA KAMA EBOLA WA IBUKA NCHINI UGANDA


Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa tahadhari ya kusafiri nchini Uganda baada ya kuthibitishwa kuwa daktari mmoja amefariki kutokana na ugonjwa hatari wa Marburg unaosambazwa na popo.Kwa sasa Shirika hilo kwa ushirikiano na mamlaka za afya za Uganda wamemzuilia ndugu mmoja wa marehemu kwa hofu kuwa huenda naye aliambukizwa. Watu wengine zaidi ya 80, wakiwemo matabibu 38 waliokutana na mwenzao huyo siku kumi kabla ya kifo chake nao pia wanachunguzwa.

Kwa mujibu wa WHO na mamlaka za afya za Uganda, matokeo ya uchunguzi katika maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Virusi kufuatia kifo cha tabibu huyo tarehe 28 Septemba yanathibitisha kwamba alifariki kutokana na homa hiyo hatari ya Marburg. Waziri wa Afya wa Uganda, Erioda Tumwesigye, alisema kuwa wizara yake inathibitisha daktari huyo aliyekuwa mtaalamu wa vipimo vya mionzi, alikufa kwa Marburg.Marehemu alikuwa tabibu katika Hospitali Kuu ya Wilaya ya Mpigi na alianza kuugua tarehe 17 Septemba akihudumu katika hospitali ya Mengo jijini Kampala, ambako alikuwa ameajiriwa mwezi mmoja uliopita. Inahofiwa kwamba katika kipindi cha wiki mbili kabla ya kifo chake alikutana na watu wengi wakiwemo matabibu wenzake pamoja na kwamba ni jamaa zake waliomzika.Kutokana na hilo, mwakilishi wa WHO nchini Uganda, Dokta Wondimagegnehu Alemu, alitahadharisha watu watu wanaoingia nchini Uganda, hasa katika wilaya ya Mpigi iliyo jirani na jiji la Kampala na pia Kasese alikozikwa marehemu. "Tunatoa tahadhari ya usafiri nchini Uganda baada ya kutambua kwamba mtu mmoja amefariki kutokana Marburg," alisema mwakilishi huyo ya WHO. Watu 80 wawekwa kwenye karantini.

Wizara ya afya ya Uganda pamoja na mashirika na taasisi nyengine husika zimechukua hatua za dharura mkiwemo kuwabaini na kuwatenga zaidi ya watu wapatao 80 waliokutana na mtu huyo aliyefariki kutokana na ugonjwa huo hatari wa Marburg.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, watu hao watachunguzwa katika kipindi cha siku 21, ambazo ndiyo muda wa ishara za ugonjwa huo kujitokeza na kubainika na "yule atakayeonesha dalili hizo atasafirishwa moja kwa moja hadi kituo cha kitaifa cha kushughulikia magonjwa hatari," alisema Daktari Jane Aceng, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Afya nchini Uganda, akiongeza kwamba wanafanya kila jitihada kuona kwamba wanamfuatilia kila mtu na "kuudhibiti ugonjwa huo mara moja kabla haujasambaa".

Popo husababisha Marburg Ugonjwa wa Marburg ni homa hatari inayonasibishwa na ugonjwa wa Ebola kwani virusi vya magonjwa hayo ni ya jamii moja ijulikanayo kama filoviridae.

Mnyama aina ya popo, ambao ni jamii ya mamalia wanaoruka na wanaoishi kwa kula matunda, ndiyo wanaosemekana kusambaza kirusi cha Marburg na maambukizi baina ya binadamu hutokana na kugusana kwa vidonda au majimaji yoyote kutoka kwa mgonjwa kama vile damu, mate, matapishi, kinyesi au mkojo wa aliyeambukizwa.

Miongini mwa dalili za ugonjwa huo ni pamoja na mtu kuwa na homa ya ghafla ya kiwango cha juu cha joto, maumivu ya kichwa, kutapika damu, maumivu ya viungo na misuli pamoja na kuvuja damu kutoka sehemu kadhaa kama vile machoni, puani, meno, masikioni, njia ya haja kubwa na hata kwenye ngozi. Aidha mtu aliyekumbwa na ugonjwa huo huharisha sana.

Kwa bahati mbaya, kama ilivyo kwa Ebola, ugonjwa huo nao haujapatiwa dawa maalum ya kuutibu wala chanjo dhidi yake. Wagonjwa hupewa tu dawa za kutuliza ishara husika.

Wataalamu wanaelezea kuwa viwango vya uwezekano wa mtu kufariki kutokana na ugonjwa huo ni kati ya asilimia 24 hadi 88, huku wakisisitiza njia za kujilinda na mgonjwa aliyekwishaathirika kuepuka kukutana kwa majimaji ya miili, damu, kinyesi au mate.

CREDIT TO: tanzaniatoday.co.tz

No comments:

Post a Comment