REDD’S Miss Tanzania Sitti Abbas Mtemvu ameamua kuvua taji la Redds Mitss Tanzania alilovikwa usiku wa Oktoba 11 mwaka huu katika Ukumbi wa Mliamani City, jijini Dar es Salaam.
Katika barua yake ya Novemba 5, kwenda kwa Kamati ya Miss Tanzania, Sitti alisema ni kutokana na shutuma dhidi yake tangu alipotangazwa mshindi wa shindano hilo.
“Mimi Sitti Abbas Mtemvu, baada ya kutwaa taji la urembo la Miss Tanzania mwaka 2014 kumezuka shutuma mbalimbali dhidi yangu, ameniwekea maneno mengi sana mdomoni kwamba nimesema wakati siyo.
“Shutuma hizo zimeandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari, Blogs na Mitandao ya Kijamii, kiasi ambacho naona inaweza hata kuhatarisha maisha yangu.
“Sasa kwa hiari yangu mwenyewe, tena bila kushawishiwa na mtu na kwa kulinda heshima yangu pamoja na familia yangu, natamka rasmi kuvua taji la urembo la Miss Tanzania 2014.
“Napenda niwashukuru wale wote waliokuwa wakinipa sapoti tangu mwanzo nilipoingia katika mashindano haya katika ngazi ya Taifa, nao ni warembo wote wa Chang’ombe, Temeke, pamoja na wote tuliokuwa nao katika fainali za Taifa.
“Pia napenda kutuma shukrani za dhati kwa waandaaji wote wa kituo cha Chang’ombe, Temeke na Wajumbe wa Kamati ya Miss Tanzania kwa mafunzo mbalimbali niliyoyapata.
“Nawashukuru pia waandishi wa habari wote kwa mchango wenu , pamoja na Wizara ya Habari , Utamaduni na Michezo na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa busara zenu.
“Leo nalivua rasmi taji nililopewa na binadamu, lakini taji alilonipa Mwenyezi Mungu, bado ninalo, mwisho naomba radhi wote kwa uamuzi huu niliouchukua.
Naye Lundenga akizungumzia uamuzi huo katika hotel ya JB Belmont alisema wamepokea barua hiyo Novemba 6 na hawana budi kuuheshimu.
Binti huyo amefikia uamuzi huo mgumu kutokana na kuandamwa kwa madai ya kudanganya umri kati ya uliopo katika nyaraka mbalimbali ikiwemo pasi ya kusafiria, leseni ya udereva na ule wa shindano hilo.
“Tumepokea barua ya Sitti, hivyo nafasi yake itachukuliwa na aliyekuwa shindi wa pili (Lilian Makazima) ambaye ni Miss Arusha na Miss Kanda ya Kaskazini,” alisema Lundenga.
Kuhusu zawadi zenye jumla ya sh. Mil 18, alisema hivi sasa ni mapema mno kujibu suala hilo hivyo taratibu za kiofisi zitafuatwa na watatoa tamko.
Kamazima alisema anafurahia kupata nafasi hiyo ya kuwa Miss Tanzania hivyo ataanza kwa kujipanga na kufanya kazi za kijamii ikiwa ni sehemu ya maandalizi yake ya kuiwakilisha nchi Miss World hapo mwakani
No comments:
Post a Comment