Saturday 8 November 2014

MISS TANZANIA SITTI MTEMVU AVUA TAJI RASMI


REDD’S Miss Tanzania Sitti Abbas Mtemvu ameamua kuvua taji la Redds Mitss Tanzania alilovikwa usiku wa Oktoba 11 mwaka huu katika Ukumbi wa Mliamani City, jijini Dar es Salaam.

Katika barua yake  ya Novemba 5, kwenda kwa Kamati ya Miss Tanzania, Sitti alisema ni kutokana na shutuma dhidi yake tangu alipotangazwa mshindi wa shindano hilo.

“Mimi Sitti Abbas Mtemvu, baada ya kutwaa taji la urembo la Miss Tanzania mwaka 2014 kumezuka  shutuma  mbalimbali dhidi yangu,  ameniwekea  maneno  mengi sana mdomoni  kwamba nimesema wakati siyo.

“Shutuma hizo zimeandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari, Blogs na Mitandao ya Kijamii, kiasi ambacho naona inaweza hata  kuhatarisha maisha yangu.
“Sasa  kwa hiari yangu  mwenyewe, tena bila  kushawishiwa  na mtu  na  kwa kulinda  heshima yangu  pamoja  na familia  yangu,  natamka rasmi kuvua  taji la urembo  la Miss Tanzania 2014.

“Napenda  niwashukuru  wale wote  waliokuwa wakinipa  sapoti tangu mwanzo nilipoingia katika mashindano  haya katika ngazi ya Taifa, nao ni warembo wote wa Chang’ombe, Temeke, pamoja  na wote tuliokuwa nao katika  fainali za Taifa.
“Pia napenda  kutuma shukrani za dhati kwa waandaaji wote wa kituo cha Chang’ombe, Temeke na Wajumbe  wa Kamati ya Miss Tanzania  kwa mafunzo mbalimbali niliyoyapata.

“Nawashukuru pia waandishi wa habari wote kwa mchango wenu , pamoja  na Wizara ya Habari , Utamaduni na Michezo na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa busara zenu.

“Leo nalivua rasmi  taji  nililopewa na binadamu, lakini taji alilonipa Mwenyezi Mungu, bado ninalo, mwisho naomba radhi wote kwa uamuzi huu niliouchukua.

Naye Lundenga akizungumzia uamuzi huo katika hotel ya JB Belmont alisema wamepokea barua hiyo Novemba 6 na hawana budi kuuheshimu.

Binti huyo amefikia uamuzi huo mgumu kutokana na kuandamwa kwa madai ya  kudanganya umri kati ya uliopo katika nyaraka mbalimbali ikiwemo pasi ya kusafiria, leseni ya udereva na ule wa shindano hilo.  

“Tumepokea barua  ya Sitti, hivyo nafasi yake itachukuliwa na aliyekuwa shindi wa pili (Lilian Makazima) ambaye ni Miss Arusha na Miss Kanda ya Kaskazini,” alisema Lundenga.

Kuhusu zawadi zenye jumla ya sh. Mil 18, alisema hivi sasa ni mapema mno kujibu suala hilo hivyo taratibu za kiofisi zitafuatwa na watatoa tamko.

Kamazima alisema anafurahia kupata nafasi hiyo ya kuwa Miss Tanzania  hivyo ataanza kwa kujipanga na kufanya kazi za kijamii ikiwa ni sehemu ya maandalizi yake ya kuiwakilisha nchi Miss World hapo mwakani

No comments:

Post a Comment